Mbunge wa jimbo la Korogwe Mjini Mary Chatanda CCM ameiambia
serikali mjini Dodoma iangalie uwezekano wa ku sheria kama zilivyo baadhi ya
nchi nyingine kwamba chama tawala kikishinda vyama vingine vitulie hadi
uchaguzi mwingine.
Bi. Chatanda ameyasema hayo katika kikao cha 45 mkutano wa
Bunge unaoendelea mjini Dodoma katika kipindi cha maswali kutoka kwa wabunge na
majibu kutoka serikalini akisisitiza kwamba kutulia kwa vyama vingine
kutawezesha chama kilichopo madarakani kutekeleza ilani yake kwa ufasaha.
Swali lake hilo likaungana na la mwenyekiti wa kamati ya
maadili na madaraka ya Bunge George Mkuchika ambaye ameiuliza serikali kwa nini
isitoe elimu kwa viongozi wa vyama vya siasa ili watambue kwamba ilani
inayotawala ni ya CCM.
Akijibu swali hilo Jenista Joakim Mhagama ni Waziri wa Sera,
Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu amesema kwamba sheria zilizopo katika
katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na utawala bora ndizo zitakazotumika
katika kuendesha shughuli mbalimbali.
Aidha Waziri Mhagama amesisitiza kwamba kama kuna haja ya
kufanya hivyo wadau watumie mchakato wa katiba unaondelea katika kufanya jambo
hilo ila kwa sasa katiba itaendelea kufuatwa kama kawaida.

0 comments:
Post a Comment